Monday, August 22, 2016

Wanaofanyiwa ukatili wa kijinsia kutibiwa bure

waziri wa afya Mh.ummy mwalimu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema agizo la serikali la kutaka kutibiwa bure kwa mtoto yeyote ambaye atakuwa amebakwa au kulawitiwa limeanza kutekelezwa rasmi.
Mhe. Mwalimu ametoa maelezo hayo leo wakati wa mapitio ya sera ya afya ya mwaka 2007 yenye lengo la kuinua hali ya afya ya wananchi wote hasa waliopo kwenye hatari zaidi kwa kuweka mfumo wa afya utakaokidhi mahitaji ya wananchi na kuongeza umri wa kuishi wa mtanzania.
Amesema utekelezaji wa agizo hilo umeanza kutumika mara moja na muuguzi yoyote atakayebainika anamtoza fedha muhanga wa vitendo hivyo atachukuliwa hatua za kinidhamu na wananchi watoe taarifa kwa haraka kwenye maeneo husika.
Wakati huohuo Waziri Mwalimu ameiagiza Taasisi ya Mifupa MOI isitishe mara moja kupeleka wagonjwa kwenda kupima vipimo vya MRI katika hospital binafsi hadi serikali itakapotoa kibali maalum cha kufanya hivyo kwa kuwa wamekuwa wanapoteza pesa za serikali kwa kuinyima mapato yake.
Aidha, akiongelea kuhusu huduma za kina mama nchini Waziri Mwalimu amesema katika kuhakikisha wanapunguza vifo vya mama na mtoto huduma hiyo inatolewa bure kwa hospitali zote za umma.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mafunzo na Maendeleo ya Wataalamu wa Afya Dkt. Otilia Gowelle amesema wizara hiyo kwa kipindi cha miaka 5 iliyopita imepunguza uhaba wa watumishi kutoka asilimia 48 hadi kufikia asilimia 51 kwa nchi nzima na vipaumbele vimewekwa kwa mikoa ambayo ina upungufu mkubwa wa watumishi kwa kushirikiana na TAMISEMI.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizari wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Mpoki Ulisubisya amesema wameweka mikakati maalum ya kuhakikisha watendaji wa afya wanafanya shughuli zao kwa uwazi na haki.
Katika utekelezaji wa sera ya afya serikali imefanikiwa kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka 5 kutoka 112 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2005 hadi 81 kwa vizazi hai 1,000 mwaka 2010 na taarifa ya kimataifa ya Septemba 2013, imeonesha Tanzania imefika lengo la milenia namba 5.

0 comments:

Post a Comment