Saturday, February 4, 2017

Yabainika: Mjane wa Tanga aliyemlilia Rais Magufuli si tapeli. Nyaraka nyeti zaibuliwa

MJANE kutoka Tanga, Swabaha Mohamed Shosi aliyewashtaki baadhi ya watendaji wa Serikali kwa Rais John Magufuli hapo jana akidai kuzungushwa kupewa haki yake ya mirathi si tapeli kama inavyosambazwa mitandaoni, FikraPevu imejiridhisha.
FikraPevu ililazimika kumtafuta Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba ili kupata ukweli wa tuhuma zilizokuwa zikielekezwa kwa mama huyo mitandaoni na aliithibitishia kuwa Jeshi lake halijawahi kupokea malalamiko yoyote dhidi ya mjane huyo kuhusika na utapeli.
Zimekuwepo jitihada za makusudi mitandaoni zikitoa taarifa zinazoonyesha kuwa kuna watu wanamfahamu kwa undani mjane huyo na kudai ni tapeli aliyekubuhu, bila kuwataja waliowahi kutapeliwa, walitapeliwa nini na lini walifanyiwa utapeli huo.
TUNACHOKIFAHAMU:
FikraPevu imepata kuziona nyaraka mbalimbali zinazohusiana na sakata la mjane huyu ikiwemo barua toka kwa Wakala wa Usajili na Ufilisi (RITA) ya tarehe 13 Februari 2014 kwenda kwa Mkuu wa Upelelezi kuwa nyaraka za ndoa ya mama huyo ni halali.
Aidha, nyaraka nyingine ni mawasiliano kati ya mjane huyo na Wizara ya Sheria na Katiba ikiwemo taarifa iliyoripotiwa Tanga kuhusu mjane kutishiwa maisha yenye RB namba TAN/IR/3371/2012.
Pamoja na hayo, hukumu ya Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Tanga chini ya Jaji P. A. Rugazia ya tarehe 3 Machi 2015 iliamuru mjane huyo asinyimwe haki yake.
KINACHOENDELEA:
Wakulyamba ameieleza FikraPevu kuwa hadi sasa Jeshi lake linayafanyia kazi malalamiko ya mjane huyo na kudai bado hajaiona taarifa inayosambazwa mitandaoni.
“Malalamiko yake mengi ni ya kweli; yapo ambayo tulimshauri aende mahakamani, na yale ya kijinai jeshi linayashughulikia katika hatua mbalimbali” aliongeza Wakulyamba katika mahojiano na FikraPevu.
Kilichotokea jana:
Katika siku ya Sheria duniani, iliyoadhimishwa kitaifa jijini Dar es Salaam jana Februari 2, mjane Swabaha alijitokeza mbele ya Rais Magufuli na kudai kuwa mhimili wa mahakama umeshindwa kumsaidia kupata haki yake ya mirathi na amekuwa akipokea jumbe za vitisho zikiwemo za kutaka kumuua ili asifuatilie mirathi yake.
Kufuatia malalamiko hayo Rais Magufuli aliwaagiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, Mkuu wa Jeshi la Polisi(IGP) Ernest Mangu pamoja na Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP) Biswalo Mganga, kuishughulikia kesi hiyo pamoja na kumpa ulinzi ili asidhurike.
Awali Swabaha alimueleza Rais kuwa mtoto wa nje ya ndoa wa marehemu mume wake, Saburia Mohamed Shosi kwa kushirikiana na Wakili wa Mahakama ya Wilaya ya Tanga, Alfred Akaro wameghushi wosia wa mumewe Mohamed Shosi kwa lengo la kumdhulumu mirathi.
Swabaha alidai kuwa, licha ya kushinda katika kesi ya mirathi aliyoifungua mwaka 2010, mahakama ilishindwa kumpa haki yake badala yake wahusika waliishinikiza mahakama hiyo kumfungulia mashitaka mapya saba.
Alisema, suala lake alilifikisha kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkuu wa Jeshi la Polisi, pamoja na Mkurugenzi wa Mashitaka na kwamba bado halijatafutiwa ufumbuzi.

0 comments:

Post a Comment