Monday, January 15, 2018

CHIRWA AFUNGIWA MECHI TATU

Mshambuliaji wa Yanga Obrey Chirwa amefungiwa kucheza mechi tatu za ligi kuu Tanzania Bara na kutozwa faini ya shilingi laki tano kwa kosa la kumpiga mchezaji wa Tanzania Prisons kwenye mchezo uliomalizika kwa sare ya kufungana bao 1-1.

Adhabu hiyo imetolewa na Kamati ya nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) iliyokutana Jumapili Januari 14, 2018 na kusikiliza kesi hiyo iliyowasilishwa na Bodi ya Ligi ikihusu mchezo namba 83 kati ya Yanga na Tanzania Prisons iliyochezwa Novemba 25, 2017 kwenye Uwanja wa Azam Complex Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa ya TFF, Chirwa alifika kusikiliza kesi hiyo akiwa na muwakilishi wake na alikiri kutenda kosa hilo.

“Kamati baada ya kumsikiliza Chirwa na kupitia video za mchezo huo pamoja na taarifa ya kamishna  na muamuzi imetoa adhabu kwa mchezaji huyo kupitia kanuni ya 37(7b) na kanuni za nidhamu za TFF kifungu cha 48(1d) na 48(2)”. Imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
@tanzania.beauty

0 comments:

Post a Comment