Na, Saed Kubenea
MBUNGE wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, amewasili salama nchini Ubegiji alikokwenda kwa matibabu.
Taarifa kutoka kwa mmoja wa maofisa wa serikali nchini humo zinasema, Lissu aliwasili kwenye uwanja wa ndege wa Zaventem, majira ya saa 11:40 ya jioni ya jana Jumamosi.
Lissu aliingia nchini humo kwa ndege ya shirika la ndege la Uholanzi (KLM), ambayo ilimchukua kutokea Amsadam, Uholanzi.
Mwanasiasa huyo machachari wa upinzani nchini, alianza safari yake ya matibabu ya tatu kutokea Nairobi, Kenya.
Aliondoka nchini Kenya kwa ndege ya shirika la ndege la nchi hiyo KQ, saa mbili asubuhi ya Jumamosi.
Kwa mujibu wa afisa huyo wa serikali nchini Ubegiji, Lissu alipokelewa uwanja wa ndege chini ya ulinzi mkali wa maofisa wa polisi na wale wa usalama.
Aidha, ulinzi umeimarishwa pia kwenye hospitali (jina tunalihifadhi kwa sasa), aliyopelekwa kwa matibabu.
Lissu alishambuliwa kwa risasi, Septemba mwaka jana akiwa nyumbani kwake Area D, mkoani Dodoma. Alikuwa akitokea bungeni alikokuwa anahudhuria mkutano wa Bunge.
0 comments:
Post a Comment